Home » » UNUNUZI WA PAMBA MWENDO WA KINYONGA

UNUNUZI WA PAMBA MWENDO WA KINYONGA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


 UNUNUZI wa pamba katika msimu wa mwaka huu Meatu mkoani Simiyu, umedorora kulinganisha na uliopita kutokana na baadhi ya kampuni zinazonunua zao hilo kudaiwa kukosa fedha ikiwamo kushindwa kukopeshwa na benki. 

Sambamba na kukosa fedha, hali hiyo inaelezwa pia inatokana na bei ya pamba katika msimu huu kuwa kubwa hatua ambayo benki zimeshindwa kuzikopesha kampuni hizo.

Msimu wa unununzi wa zao hilo uliozinduliwa rasmi kitaifa Juni 05, mwaka huu katika kijiji cha Mwabusalu wilayani Meatu kwa bei elekezi ya Sh. 1,200 kwa kilo na jumla ya kampuni 14 zilikamilisha maadalizi ya awali ya ununuzi wa zao hilo.
Akizungumza na Nipashe juzi, Mkaguzi wa Pamba katika wilaya ya Meatu, Renatus Philbert, alisema kutokana na kudorora huko, baadhi ya kampuni zimeanza kufunga vituo vya ununuzi na kusababisha kususa kwa baadhi ya vijiji wilayani humo.

Alisema pamoja na kampuni hizo 14 kukamilisha maadalizi muhimu ya ununuzi, 12 kati ya hizo ziliingia sokoni na kuanza kununua pamba lakini zikakabiliwa na ukosefu wa fedha hivyo kushindwa kuendelea na mchakato huo.

Philbert alisema kutokana na hali hiyo, baadhi ya kampuni zimekuwa zikiwakopa wakulima huku zinapodaiwa kulipa fedha zimekuwa zikishindwa huku baadhi ya maofisa wakidaiwa kutoa lugha zisizo na staha kwa wakulima.

Pamoja na kusuasua kwa ununuzi huo, alisema baadhi ya wakulima walioko kwenye kilimo cha mkataba na uzalishaji wa mbegu, hawajaathirika kwa kuwa kampuni walizoingia nazo mkataba bado zinawapelekea fedha licha ya kusitisha ununuzi kwa baadhi ya vituo vilivyo nje ya kilimo cha mkataba.

Licha ya kuwapo kwa hali ya kusuasua, alisema baadhi ya kampuni ikiwamo Kampuni ya BioRe (T) Ltd ya Meatu, imeonyesha kumudu vyema kununua pamba inayolimwa kutokana na kilimo hai katika vituo vyake vyote 16. Alisema kampuni hiyo inanunua na kulipa fedha taslimu na kusafirisha hadi kiwandani kwa kuzingatia kanuni za zao hilo.

Chanzo:Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa