Home » » Simiyu tayari kujenga kiwanda cha bidhaa za afya

Simiyu tayari kujenga kiwanda cha bidhaa za afya

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


MKOA wa Simiyu umedhamiria mwaka huu kuanza kujenga kiwanda cha aina yake Afrika Mashariki cha kutengeneza bidhaa za afya zinazotokana na pamba baada ya hatua za upembuzi yakinifu kuelekea kukamilika na michoro ya ramani ya kiwanda kuthibitishwa.
Akizungumza jana, siku moja kabla ya Jukwaa la biashara kufanyika mkoani hapa leo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, alisema hatua hiyo, siyo tu kwamba inalenga kutekeleza mpango wa kujenga Tanzania ya viwanda, lakini pia itasaidia katika kuongezea thamani ya zao la pamba.
Mkoa wa Simiyu ndio unaotoa asilimia 60 ya pamba yote inayolimwa Tanzania kwa mujibu wa takwimu za mwaka huu.
“Simiyu tunaongoza kwa kuzalisha pamba nchini, lakini unajiuliza tuna sababu gani ya hii nchi kuagiza pamba za kusafisha masikio, tuna sababu gani ya kuagiza bandeji, kuagiza pampasi, kuagiza taulo za usafi wa akina mama, tuna sababu gani ya kuagiza pamba za kusafishia vidonda? Hatuna sababu hiyo,” alisema.
Alisema walikaa na kuona ili wazo la kuanzisha kiwanda hicho kitakachogharimu takribani Sh bilioni 250 lisibaki nadharia wakaamua kushirikisha wadau na sasa linaelekea kuwa kitu halisi.
Baada ya mkoa kutoa ardhi, Mtaka alitaja wadau wanaoshiriki katika kiwanda hicho kitakachokuwa pia kinazalisha maji yanayotumika hospitalini kwa kuwaongeza wagonjwa (dripu) kuwa ni Shirika la Bima ya Afya (NHIF) litalogharimia ujenzi huku Bohari la Dawa (MSD) likitazamiwa kuwa mnunuzi mkuu wa bidhaa hizo.
Katika ujenzi huo alisema fedha zinatazamiwa kutolewa na Benki ya TIB huku Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) vikihakikisha kiwanda kinatoa bidhaa zenye wezo wa kushindana kimataifa.
Wadau wengine katika mradi huo, Mtaka aliwataja kuwa ni Taasisi ya Utafiti wa Viwanda na Maendeleo (TIRDO), Shirika la Uhandisi, Usanifu na Uzalishaji Bidhaa Tanzania (TEMDO), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).
“Tunatamani kuona Rais John Magufuli atakapokuwa anasimama mwaka 2020 kuomba tena ridhaa ya Watanzania kuongoza nchi anasema baada ya ujenzi wa hospitali na zahanati, sasa pia tumeanza kujitosheleza kwenye biadhaa za hospitali zinazozalishwa kwa pamba,” alisema.
Akiongelea kuhusu jukwaa la uchumi linalofanyika leo mkoani hapa, Mtaka aliwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kuja Simiyu kuwekeza na kutumia vyema sera ya wilaya moja bidhaa moja.
Jukwaa hilo lililoandaliwa na TSN, wachapishaji wa magazeti ya HabariLeo na Daily News naSpotiLeo, kwa kushirikiana na Mkoa wa Simiyu, linawakutanisha pia wadau muhimu wa maendeleo kama vile vyombo vya fedha; Benki za TIB na NMB, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa