Home » » Morali ya ufundishaji yaongezeka shule ya Msingi Igaganulwa

Morali ya ufundishaji yaongezeka shule ya Msingi Igaganulwa

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na. Lilian Lundo – MAELEZO - Simiyu

Morali ya ufundishaji wa walimu wa shule ya Msingi Igaganulwa iliyoko kata ya Dutwa, Halmashauri ya Wilaya ya Baridi Mkoani Simiyu umeongezeka na kupelekea shule hiyo kuwa na ufulu wa juu wa wahitimu wa darasa la Saba mwaka 2016.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Robert Majani aliyasema hayo Wilayani Bariadi wakati wa Mahojiano na timu inayosimamia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu ya Wilaya hiyo kuhusu maendeleo ya taaluma ya shule yake.

“Miaka mitatu iliyopita morali ya ufundishaji wa walimu wa shule hii ilikuwa ya chini kutokana ushirikiano hafifu uliokuwepo kati ya walimu wakuu wa miaka ya nyuma na walimu wa shule hii, tatizo hilo  lilipelekea walimu kuondoka  kwenye vituo vya kazi kabla ya muda wa kazi  kumalizika pamoja na  utoro uliokithili kwa wanafunzi,” alifafanua Mwalimu Majani.

Aliendelea kwa kusema kuwa, kulikuwa hakuna uwazi wa mapato na matumizi ya fedha za shule baina ya uongozi wa shule, walimu wa shule hiyo na wadau wa elimu. Vile vile kulikuwa na upungufu wa vitendea kazi pamoja na samani za ofisini hivyo walimu kufanya kazi katika mazingira magumu.

Tatizo hilo la walimu katika shule hiyo lilipelekea ufaulu wa chini pamoja na utoro uliokithili kwa wanafunzi kutokana na kutokuwepo kwa uangalizi wa walimu hivyo wanafunzi walikuwa wakienda shule pale wanapopenda.

Katika kurudisha morali ya walimu wa shule hiyo Mwalimu Majani  kupitia vikao vya kamati ya taaluma, walimu wakorofi walikoselewa ili kurekebisha tabia, pia  kamati ya shule iliunda sungusungu ambao walikuwa wakiwakamata na kuwarudisha shuleni wanafunzi wanaotoroka shule.

Vile vile walimu walibadilishiwa masomo ya kufundisha baada ya kuonekana baadhi ya walimu wa masomo ya ufundi kutofanya vizuri katika masomo hayo hivyo wakapewa masomo ambayo wanayamudu kufundisha.

Mapato na matumizi ya fedha ya shule hiyo vimewekwa wazi kwa walimu wote pamoja na kushirikishwa katika upangaji wa bajeti ya shule hiyo.

Aidha Mwalimu Majani ameanzisha programu ya kutoa chai kwa walimu wa shule hiyo kwa kutumia posho yake ya madaraka ambapo imesaidia kupunguza muda wa walimu kwenda kunywa chai mjini ambako ni mbali na shule.

Mabadiliko hayo yamepelekea kuongezeka kwa hamasa ya walimu kufundisha hivyo kupandisha ufaulu wa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba ambapo kwa mwaka 2016 shule hiyo imeshika nafasi ya Sita Kiwilaya  kutoka nafasi ya 28 mwaka 2015.

Mwalimu Majani alisema kuwa sababu nyingine iliyoipelekea shule hiyo kufanya vizuri zaidi mwaka huu 2016 ni pamoja na mafunzo yanayotolewa na Serikali kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Nchini (Education Quality Improvement Programme-Tanzania) EQUIP-T ambapo walimu wamekuwa wakipata mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kuwapa motisha ya kazi.

Mwisho

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa